Marekani, EU na AU wamshutumu Odinga kwa ‘kujiapisha’ Kenya

Written by on February 2, 2018

Serikali ya Marekaniimesema imesikitishwa na hatua ya kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ya kujiapisha Jumanne wiki hii.

Marekani pia imeishutumu serikali kwa kufungia vituo vinne vya habari nchini humo ambavyo viliadhibiwa baada ya kupeperusha moja kwa moja hafla hiyo ya upinzani.

Umoja wa Afrika na Muungano wa Ulaya pia wameshutumu hatua hiyo ya Bw Odinga.

Kupitia taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema taifa hilo linaamini mizozo yoyote ile inafaa kutatuliwa kwa njia zifaazo kisheria.

“Tunakataa vitendo vyovyote ambavyo vinahujumu Katiba ya Kenya na utawala wa sheria. Uhuru Kenya alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya mnamo Oktoba 26, 2017 katika uchaguzi ambao uliidhinishwa na Mahakama ya Juu,” taarifa hiyo iliyotumwa na msemaji wa wizara hiyo Hearther Nauerth imesema.

“Umoja wa Afrika unakataa vitendo vyote amabvyo vinahujumu mfumo wa kikatiba na utawala wa sheria. Mwenyekiti wa Tume (Moussa Faki Mahamat) anatoa wito kwawahusika wote kujiepusha na vitendo kama hivyo ambavyo pia vinatia hatarini uthabiti wa kisiasa Kenya,” taarifa ya Tume ya Umoja wa Afrika imesema.

Bw Odinga, mgombea urais wa muungano wa National Super Alliance (NASA) uchaguzi wa tarehe 8 Agosti ambao matokeo yake yalibatilishwa baada ya kesi iliyowasilishwa naye Mahakama ya Juu, alisusia uchaguzi huo wa marudio na amesema hamtambui Rais Kenyatta kama rais halali wa taifa hilo.

Jumanne, alikula kiapo kuwa Rais wa Wananchi katika hafla iliyohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake uwanja wa Uhuru Park, Nairobi.

Mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, ambaye ni makamu wa rais wa zamani, hakuhudhuria sherehe hiyo ingawa walikuwa wameahidi kuapishwa wote wawili kwa pamoja.


Reader's opinions

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *


Clouds FM

The People's Station

Current track
TITLE
ARTIST

Background